Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s)-ABNA-;Sheikh Naim Qasim, akizungumza na kituo cha televisheni cha Al-Manar, alisema:
“Kuna uwezekano wa vita, lakini si jambo lililothibitishwa; yote yanategemea maamuzi ya adui wa Kizayuni (Israeli) kulingana na hali ya kijeshi ilivyo. Hatuwezi kufanya chochote zaidi ya kuwa tayari kwa uwezekano huo.”
Aliongeza kuwa Israel haiwezi kufikia malengo yake nchini Lebanon, na kwamba:
“Iwapo vita vitatulazimishwa, hata kama tutakuwa na kipande kimoja cha mbao, hatutaruhusu Mzionisti yeyote avuke. Tutapigana hadi mwisho – awe mwanaume au mwanamke.”
Sheikh Qasim alisema kuwa leo hii, Hezbollah imekuwa imara zaidi kuliko kabla ya vita vya ‘Awwalul Ba’s’, na kwamba kuna ongezeko la nguvu, uimara, heshima, na azma ya kuendelea mbele.
“Msingi wa kuendelea kwa muqawama ni imani na irada. Silaha na idadi ya wapiganaji ni nyongeza tu kwenye imani hiyo,” alisema.
Akaongeza kuwa muqawama wa Lebanon ni harakati ya kitaifa, ingawa unafanya kazi zaidi katika jamii ya Kishia, lakini unawakilisha madhehebu yote na ni kwa ajili ya taifa zima la Lebanon.
“Kuwa na Silaha ni Haki Yetu ya Kisheria”
Akijibu madai kuhusu kuweka silaha zote mikononi mwa serikali, Sheikh Qasim alisisitiza kuwa:
“Kuwa na silaha ni sehemu halali na isiyotenganishwa na haki yetu ya kujilinda na kulinda uwepo wetu. Kati ya sisi na nchi yetu hakuna tofauti.”
Alibainisha kuwa uwepo wa kijeshi wa Hezbollah unahusiana moja kwa moja na uwepo wa adui mnyakuzi wa Kizayuni, na kwamba jukumu la muqawama halijaisha, kwani uvamizi bado unaendelea.
Aliongeza:
“Jeshi la Lebanon linapaswa kukabiliana na uvamizi, na pale ambapo haliwezi kutekeleza jukumu hilo, basi wananchi wenye roho ya upinzani ndio watakao simama kupambana.”
Kwa mujibu wa Sheikh Qasim, Hezbollah ipo tayari kushirikiana na serikali na jeshi la Lebanon kuunda mkakati wa kitaifa wa ulinzi unaolenga kulinda nchi.
Alisisitiza kuwa jeshi la Lebanon ni la kitaifa, linafikra za kitaifa, na limekuwa likifanya kazi vizuri katika kipindi cha nyuma na sasa.
“Jeshi limeweza kupata ridhaa ya wananchi, na hali hiyo inapaswa kudumishwa,” alisema.
“Serikali Inapaswa Kuwajibika Zaidi Dhidi ya Uvamizi wa Israel”
Kuhusu mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya Lebanon, Sheikh Qasim alisema:
“Serikali ya Lebanon inapaswa kuwa na msimamo mkali zaidi dhidi ya uvamizi huu, na tunaitaka ifanyie marekebisho kamati inayohusika na ufuatiliaji wa uvamizi.”
Kuhusu ujenzi upya (reconstruction) wa maeneo yaliyoharibiwa, alisema:
“Wajibu wa ujenzi wa upya uko mikononi mwa serikali. Mvamizi ni Israel, na Lebanon ndiyo iliyoshambuliwa. Serikali inapaswa kuanza haraka mchakato wa ujenzi – si miundombinu pekee bali ujenzi kamili wa taifa. Ianzishe mfuko maalum, itafute msaada wa kimataifa, na itumie rasilimali zake.”
Kuhusu Wafungwa na Uhusiano na Saudi Arabia
Sheikh Qasim alisema kuwa jukumu la kwanza kuhusu wafungwa wa Kilebanon liko mikononi mwa serikali, na ni lazima ishughulikie suala hilo kwa nguvu zaidi.
Kuhusu pendekezo lake la kufungua ukurasa mpya na Saudi Arabia, alisema:
“Hatujapokea mwitikio wowote. Hakuna aliyezungumza nasi kuhusu hilo. Ikiwa dalili chanya zitatoka upande wa Saudi Arabia, tutalipokea vizuri. Tumeeleza wazi kuwa Hezbollah ipo tayari kwa mazungumzo na imefungua mikono yake kwa wote.”
Uchaguzi wa Bunge Kufanyika kwa Wakati Uliopangwa
Sheikh Qasim alisisitiza kwamba Hezbollah inaunga mkono kufanyika kwa uchaguzi wa bunge kwa wakati uliopangwa, bila ucheleweshaji wowote.
“Hatuna ajenda maalum; sheria ipo, basi itekelezwe,” alisema.
Kuhusu muungano wa kisiasa, alibainisha kuwa:
“Tutafanya muungano pale tu ambapo kuna maslahi ya kisiasa au ya uchaguzi.”
Mahusiano na Waziri Mkuu Nauf Salam
Akizungumzia uhusiano na Waziri Mkuu Nawaf Salam, Sheikh Qasim alisema:
“Kuna tofauti za maoni katika baadhi ya mambo, lakini si tatizo. Tunataka mafanikio ya serikali na umoja wa taifa.”
Aliongeza kwa ujumbe maalum kwa Waziri Mkuu:
“Tuko tayari kushirikiana nawe kwa nia njema. Hatuwezi kukubaliana na mambo yanayoweza kusababisha mgogoro wa kitaifa, lakini tupo tayari kwa majadiliano ya kibinafsi kufikia makubaliano ya pamoja kwa ajili ya mafanikio ya nchi.”
Your Comment